Wafuasi wa Chadema mjini Nansio Wilaya ya Ukerewe, Mwanza wakishangilia ushindi katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika juzi. Picha na Jovither Kaijage |
Hayo yanaonyesha kuwa vyama hivyo vimeanza
kuimarika katika ngazi za chini, tofauti na ilivyokuwa mwaka 2009,
katika uchaguzi ambao CCM kilipata ushindi wa kishindo wa asilimia
91.72, huku wapinzani wakigawana asilimia 8.28 zilizobaki.
Licha ya uchaguzi wa juzi kugubikwa na kasoro
lukuki, upinzani umeonekana kuchomoza huku katika baadhi ya mikoa
ukipata ushindi maradufu hasa katika ile ambayo una nguvu kubwa wakati
katika maeneo ambayo ulikuwa na viti vichache au kutokuwa navyo kabisa,
umeibuka na kuipokonya CCM baadhi ya mitaa na vijiji.
Vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa); Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi vimejizolea viti vingi tofauti na
awali, huku chama kipya cha ACT kikichomoza na kupata ushindi katika
maeneo kadhaa ya mikoa ya Kigoma na Katavi.
Mikoa ambayo upinzani umeonekana kuzoa viti vingi
ni Arusha, Kilimanjaro, Mbeya, Iringa, Kigoma, Mara, Kagera na Dar es
Salaam, hali ambayo wachunguzi wa mambo wameielezea kuwa siyo dalili
njema kwa CCM.
Nguvu ya upinzani inaonekana kuongezeka siku hadi
siku ikilinganishwa na ilivyokuwa mwaka 1995 wakati ulipofanyika
Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama vingi vya siasa.
Hii ni mara ya kwanza kwa vyama vya upinzani
kuonyesha ushindani mkubwa katika uchaguzi wa chini, hali ambayo inaweza
kuwa ni jibu la ukosoaji ambao umekuwa ukifanywa kwamba vyama hivyo
vimejikita mjini tu na kusahau kufanya siasa kwa wananchi.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Ruco) Iringa,
Profesa Gaundence Mpangala alisema matokeo ya uchaguzi yanayoendelea
kutangazwa, yanadhihirisha kuwa CCM itaendelea kukabiliwa na upinzani
mkubwa hata kwa Uchaguzi Mkuu ujao mwakani.
Licha ya mafanikio hayo, kwa upande wa upinzani,
matokeo ya jumla yanaonyesha kuwa bado CCM inaelekea kushinda kwa kupata
mitaa na vijiji vingi ikilinganishwa na upinzani.
CCM kinaendelea kuweka mizizi katika mikoa ya
Tanga, Morogoro, Dodoma, Pwani na baadhi ya wilaya katika mikoa ya
Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Mbeya, Iringa na Mwanza.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni