promotion

Jumatatu, 15 Desemba 2014

Simu kutumika taarifa za magonjwa ya mlipuko



Wizara ya Afya, na Ustawi wa Jamii, itaanza kutumia mfumo mpya wa utoaji wa taarifa za magonjwa ya mlipuko kwa kutumia simu za mkononi kwa lengo la kuyadhibiti mara yanapogundulika kabla ya kusababisha madhara makubwa.
Naibu katibu mkuu wa Tamisemi, Dk Deo Mtasiwa alisema hayo jana katika mkutano ulioshirikisha wataalamu wa magonjwa ya binadamu na wanyama pamoja na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) ili kuangalia njia itakayotumika kurahisisha upatikanaji wa taarifa hizo.
Alisema mfumo wa kushughulikia magonjwa ya mlipuko ya kuambukiza kwa binadamu na wanyama katika nchi za Afrika bado ni hafifu na kuwapo kwa mfumo huo wa kutumia mawasiliano ya simu kutoka kwa wagonjwa kwenda kwa wataalamu kutarahisisha udhibiti wa magonjwa hayo kwa haraka.
Alisema kitendo cha wataalamu wa Afrika kupitisha uamuzi wa kutumia teknolojia hiyo, kutasaidia kupiga hatua.
na kuwa mfano wa kuigwa.
“kwa kweli sisi kama Serikali kupitia Wizara ya Afya, mfumo huu tunautumia katika kipengele cha matokeo makubwa sasa (BRN) katika kuuboresha na kuufanyia kazi kwa ngazi ya kimataifa ili Tanzania katika nchi za Afrika uwe ndiyo mfano wa kuigwa na nchi zingine kwa kufanya vizuri kupitia mfumo huu,” alisema Dk Mtasiwa.
Mtafiti kutoka SACIDS, Profesa Esron Karimuribo alisema kwa pamoja wameweza kukutana na wataalamu hao ili kuangalia njia itakayotumika kurahisisha upatikanaji wa taarifa hizo zitakazosaidia kuzuia vifo vinavyotokea pindi magonjwa hayo yanapozuka.
Alisema kupitia mfumo huo wa mawasiliano, taarifa za magonjwa hayo zitaifikia Serikali na wataalamu wake kwa haraka ili wachukue tahadhari kabla ya kuleta madhara kwa jamii.
Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine, Kadeghe Fue alisema kabla ya kuwapo kwa mfumo huo, taarifa zilikuwa zikichelewa kuwafikia wataalamu kwa kuwa walikuwa wakitumia makaratasi na sasa kwa kutumia teknolojia ya mawasiliano ya simu za mkononi itaharakisha upatikanaji wa taarifa hizo na zitasambaa kwa wakati.

Hakuna maoni: