promotion

Jumatatu, 17 Novemba 2014

Wizara ya Afya wakaidi amri ya mahakama





WATENDAJI wa Wizara ya Afya wameingia katika mgogoro na mhimili wa mahakama baada ya kukaidi amri ya kukifungulia kituo cha tiba za asili na mbadala cha Foreplan Herbal Clinic.
Kituo hicho kilifungwa Novemba 6 mwaka huu, baada ya watendaji wa wizara hiyo kufanya ukaguzi.
Kwa mujibu wa mmliki wa kituo hicho, Dk. Juma Mwaka, Novemba 7 mwaka huu, alifungua kesi ya madai katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala dhidi ya Baraza la Tiba Asili na Mbadala, pamoja na maofisa tisa kutoka wizarani walioshiriki ukaguzi.
Kesi hiyo ilifunguliwa na mawakili wa Dk. Mwaka, ambao ni Lucas Kamanija na Ngassa Mboje, kutoka kampuni ya mawakili ya Kamanija and Company Advocates.
Walioshtakiwa ni Mboni Bakari, Dk. LiggleVumilia, Dk. Mahewa Lusinde, Vera Ndechilio, Sophia Ntomole, John Chilomo, Laura Marandu na Dk. Jacqueline Kiloji.
Kwa mujibu wa mmliki wa kituo hicho, kesi hiyo ya msingi ilipewa namba 204 ya mwaka 2014 na mawakili wake pia waliwasilisha maombi madogo Namba 349 ya mwaka 2014 katika mahakama hiyo hiyo ya Wilaya ya Ilala.
Maombi hayo waliyawasilisha chini ya hati ya dharura, wakiomba wasikilizwe upande mmoja na wapewe amri kwamba washitakiwa wakafungue majengo ya Kliniki ya Dk. Mwaka.
Mawakili wa Dk. Mwaka, waliomba pia mahakama iwaamuru washtakiwa wakafute maandishi waliyoyaandika kwenye kuta za kliniki hiyo yanasosomeka; ‘Kituo hiki kimefungwa na Wizara ya Afya leo 06/11/1914’.
Pia walitaka washitakiwa wasiingilie biashara ya Dk. Juma Mwaka mpaka kesi itakaposikilizwa pande mbili.
Mahakama hiyo ya Wilaya ya Ilala, ilikubaliana na maombi hayo madogo ya Dk. Juma Mwaka na ikawaamuru washitakiwa wakafungue majengo ya Kliniki hiyo na wasiingilie biashara ya mdai hadi kesi itakaposikilizwa pande mbili.
Kwa mujibu wa taarifa ilizozipata Tanzania Daima, washitakiwa walipelekewa amri hizo kupitia Ofisa wa Mahakama Novemba 10 lakini hawakuzipokea.
Inadaiwa kutokana na kitendo hicho cha washtakiwa, Novemba 11 mwaka huu mawakili wa Dk. Mwaka walirudi tena mahakamani na wakawasilisha maombi madogo chini ya hati ya dharura kuiomba mahakama itoe hati ya kuwakamata washitakiwa.
Mawakili hao walitaka washtakiwa waieleze mahakama kwanini wasiadhibiwe kwa kosa la kuidharau mahakama
Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala, aliyetambulika kwa jina la Msafiri, alitoa amri ya kukamatwa kwa washitakiwa na uamuzi huo ulikabidhiwa kwa polisi ili wautekeleze.
Hata hivyo, inadaiwa polisi imeshindwa kuwakamata washitakiwa huku lawama zikielekezwa kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP), Mary Nzuki anayedaiwa kukalia amri hiyo.
Tanzania Daima, iliwasiliana na Kamanda Nzuki, ambaye alisema hajapata amri hiyo.
Kwa upande wake, Msemaji wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Nsachris Mwamwaja, alisema hana taarifa kamili juu ya jambo hilo na akataka atafutwe Mwenyekiti wa Baraza la Tiba Asili na Mbadala.
“Nawaombeni kesho tuonane ofisini niweze kuwapeleka kwa wahusika kwa kuwa anayehusika na zoezi la kufungia vituo vya tiba asili na mabadala visivyokidhi vigezo vinavyotakiwa ni Mwenyekiti wa Baraza,” alisema.

Hakuna maoni: