WAKAZI wa Wilaya ya Momba mkoani Mbeya wamempongeza Mbunge wao David Silinde (CHADEMA) kwa kutimiza ahadi ya kuondoa tatizo sugu la maji aliyoitoa mwaka 2010 wakati wa kampeni.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Tanzania Daima iliyotembelea jimbo hilo, walisema mbunge wao ni chachu ya maendeleo baada ya kutatua kero lukuki ikiwemo ya ujenzi wa visima vinne vya maji safi vyenye thamani ya sh milioni 1.2.
Husein Saidi mkazi wa Tunduma alisema tatizo la maji liliwaweka wajawazito na wanawake wa Momba katika hatari ya kubakwa na kujifungulia barabarani wakitafuta maji.
Christina Njoka alisema mbunge huyo ni mfano wa kuigwa kwa kuwa yupo karibu na wapigakura wake wakitekeleza ahadi.
“Tupo tayari kumuunga mkono Silinde kupitia CHADEMA ili aendelee kutuongoza kwa muhula wa pili kwa kuwa tumeona matunda aliyotuletea ya kuondoa changamoto zetu… sasa tunaanza kwa kuwachagua wenyeviti wa mitaa,” alisema Njoka.
Silinde alisema anafarijika kuona wananchi wakipongeza harakati zake jambo linalompa nguvu na kuamini kwamba ataendelea kuwa mbunge wa Momba kwa kipindi kijacho.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni