MKURUGENZI
WA SERIKALI ZA MITAA BWANA KHALIST LUANDA AKIZUNGUMZA NA WAANDISHI WA
HABARI (HAWAPO PICHANI) JUU YA KUKAMILIKA KWA MAANDALIZI YA UCHAGUZI WA
SERIKALI ZA MITAA MJINI DODOMA LEO AMBAPO ALITANGAZA RASMI TAREHE YA
KUANDIKISHA KUPIGA KURA . (PICHA NA HABARI KUTOKA OFISI YA WAZIRI MKUU
TAMISEMI).
|
Mkurugenzi
wa Serikali za Mitaa katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na
Serikali Mitaa Bwana Kharist Michael Luanda amesema wananchi
wanapaswa kujiandikisha katika daftari maalum la kupigia kura kwa ajili
ya kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa kuanzia tarehe 23/11/2014
hadi tarehe 29/11/2014.
Mkurugenzi
huyo alisema kuwa wananchi wanaotaka kugombea nafasi mbalimbali za
uongozi katika ngazi za vijiji, vitongoji na mitaa wanapaswa kuchukua
fomu za kugombea kuanzia tarehe 16/11/2014 hadi tarehe 22/11/2014.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma, Bwana Luanda aliwataka
wananchi kujitokeza kwa wingi katika zoezi la kujiandikisha ili waweze
kupata fursa ya kushiriki katika kupiga kura ili kuwachagua viongozi wa
vijiji, vitongoji na mitaa wanaowataka.
Alisema
sifa za mtu anayestahili kujiandikisha kushiriki uchaguzi huo ni lazima
awe raia wa Tanzania, mwenye umri wa miaka 18 au zaidi, mkazi wa eneo
hilo na mwenye akili timamu.
Pia
alisisitiza kuwa uandikishaji huo utafanyika katika vituo maalum
vilivyoandaliwa ambavyo vipo katika majengo ya umma, isipokuwa sehemu
ambazo hazina majengo hayo, uandikishaji utafanyika katika vituo maalum
kutokana na makubaliano ya Msaidizi wa Uchaguzi na viongozi wa vyama vya
siasa.Bwana Luanda amesisitiza kuwa vituo hivyo vitafunguliwa saa 1:30
asubuhi na kufungwa saa 10:30 jioni.
Aidha alisema kuwa vyama vya Siasa vitaruhusiwa kuweka mawakala wao wakati wa uandikishaji wa wa wapiga kura lakini gharama za kuwalipa zitakuwa juu ya chama husika. Kuhusu sifa
za mtu anayetaka kugombea nafasi mbalimbali katika ngazi ya vitongoji,
vijiji na mtaa Mkurugenzi huyo alisema kuwa ni lazima awe mtanzania mwenye umri wa miaka 21 au zaidi na awe mkazi wa kudumu wa eneo husika.
Vile vile alisema kuwa wasimamizi wasaidizi wa kila kituo wanapaswa kubandika
orodha ya wapiga kura tarehe 30/11/2014, endapo mkazi yeyote au chama
cha siasa kitakuwa na pingamizi au maoni juu ya orodha hiyo basi
awasiliane na msimamizi msaidizi wa uchaguzi ili kuweza kufanyia
marekebisho na orodha ya mwisho itabandikwa siku tatu kabla ya uchaguzi.
Uchaguzi
wa serikali za Mitaa Tanzania Bara umepangwa kufanyika disemba 14,
2014, ambapo wananchi watawachagua wenyeviti wa vijiji, vitongoji,
Mitaa, Wajumbe wa Halmashauri za vijiji na Wajumbe wa Kamati za Mitaa.
Viongozi
watakaochaguliwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa ni pamoja na
wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji wasiopungua 15 na wasiozidi 25,
wenyeviti wa Mitaa na wajumbe wa kamati za Mitaa wasioziidi 6 na
wenyeviti wa vitongoji wa kila kitongoji.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni