promotion

Alhamisi, 20 Novemba 2014

MADIWANI MASWA WAIANGUKIA SERIKALI







Na Samwel Mwanga-Maswa

MADIWANI wa halmashauri ya wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu wameiomba
Serikali kupitia Wizara ya Kilimo,Chakula na Ushirika kukamilisha
mradi wa kilimo cha Umwagiliaji wa zao la Mpunga ulioko katika kijiji
cha Kinamwigulu wilayani humo ili wananchi wanufaike nao.

Ombi hilo limetolewa jana katika kikao cha Baraza la Madiwani
kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri  hiyo ulioko mjini
Nyalikungu.

Walisema kuwa pamoja na kazi nzuri inayofanywa na serikali ya kutoa
fedha kwa ajili ya utekelezaji shughuli mbalimbali za maendeleo kama
ulivyo mradi huo ni vizuri ikatoa fedha  ili ukamilike na wananchi
wanufaike na matunda yake.

“Serikali kwa kweli inafanya kazi nzuri ya kutoa fedha ili kutekeleza
miradi mbalimbali kama ulivyo Mradi huu wa umwagiliaji wa Kinamwigulu
hivyo basi tunaomba iongeze kasi ili kazi hii ikamilike na wananchi
wafurahie matunda ya kazi hiyo”Alisema Slivanus Mipawa,diwani wa  Kata
ya Buchambi.

Walisema kuwa mradi huo umekuwa ukisuasua kutokana na ukosefu wa fedha
hali ambayo imemfanya mkandarasi aliyepewa kujenga Skimu hiyo kusimama
kwani hadi sasa ni kiasi cha Shilingi 69,818,998/=ndizo zilizotolewa
kati ya Shilingi 698,189,988/=sawa na asilimia 10.

Naye Ofisa Kilimo,Ushirika na Umwagiliaji wilaya ya Maswa,Thomas
Shilabu alisema kuwa Skimu hiyo yenye ukubwa wa Hekta 64.6 huku eneo
la Hekta 250 ndizo zinazofaa kwa kilimo cha Umwagiliaji zitazinufaisha
Kaya zipatazo 78.

Shilabu alisema kuwa ujenzi wa Skimu hiyo umekuwa ukisimamiwa moja kwa
moja na Wizara na hivyo kuiomba serikali ili halmashauri ya wilaya
hiyo iweze kuusimamia na Wizara ya Kilimo,Chakula na Ushirika wawe
wakaguzi.

“Changamoto kubwa ya Mradi huu ni kwamba unasimamiwa na wizara sisi
halmashauri ya wilaya hatuhusiki kabisa ila mie nashauri Wizara
ituachie tuusimamie siye Halmashauri ya wilaya ya Maswa ilete fedha
kwetu na wao wabaki kuwa wakaguzi wa shughuli hiyo  nina imani
utakamilika kwa wakati”Alisema.



Hakuna maoni: