promotion

Alhamisi, 27 Novemba 2014

Mulongo aingia Mwanza na gia ya machinga

Mkuu mpya wa mkoa wa Mwanza,Magesa Mulongo.



Mkuu mpya wa mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo (pichani), ameitaka halmashauri ya jiji la Mwanza kutotumia nguvu kuwadhibiti machinga na badala yake kukaa pamoja ili wasiichukie serikali.

Akizungumza katika kikao cha kujitambulisha kwa uongozi wa mkoa wa Mwanza jana, Mulongo alisema kutumia nguvu kuwatimua machinga katika sehemu wanazofanyia biashara,  kunazalisha chuki na serikali pamoja na wale walioharibiwa mali zao.

“Hawa machinga kuweni karibu nao kwani si wakimbizi, msiite jeshi kukabiliana nao bali mkae na kuelewana nao jinsi gani ambavyo wataweza kulipa kodi…kusanyeni mapato kwao na kwa bodaboda lakini kwa kufanya mipango thabiti,” alisema Mulongo.

Mulongo ambaye kabla ya kuripoti mkoa wa Mwanza, alikuwa mkuu wa mkoa Arusha alikohamishiwa Evarist Ndikilo aliyekuwa mkoani hapa.

Alisema lazima halmashauri zote za mkoa wa Mwanza hususani ya Jiji kuhakikisha linakuwa salama na madeni wanayodaiwa kuyamaliza.

“Wekeni utaratibu wa ukusanyaji mapato kwa wahusika ili msishindane na mitutu…kusanyeni mapato kwa mipango,” alisema.

Aidha, alilitaka Jiji hilo kutowaahidi machinga kwamba wanawapeleka sehemu ya kufanyia kazi yenye neema, wakati si kweli hali ambayo inaweza kusababisha kurejea tena sehemu waliyotolewa.

Mkuu huyo wa mkoa akielezea kuhusu maabara, alisema halmashaauri itakayolea ujinga na kushindwa kukamilisha maabara, zihakikishe zinawajibika.

“Wakurugenzi wasimamie suala la maendeleo la halmashauri zao ili msiziue kwa kisingizio cha kutoziona nakala husika,” alisema.

Hata hivyo, aliwataka watendaji wa mkoa huo kutimiza wajibu wao na wala wasitegeane kufanya kazi na lazima taarifa zifikishwe kwa wakurugenzi kila siku za kazi.

Mkutano huo wa utambulisho ulihudhuriwa na wakuu wa wilaya zote, wakurugenzi, wenyeviti wa halmashauri na mameya wa Jiji hilo.
 

Hakuna maoni: