promotion

Jumanne, 25 Novemba 2014

MSANII JB BONGE LA BWANA KUFUNGA MWAKA NA ‘MZEE WA SWAGA’..MCHEKI HAPA



Ni staa asiyeonekana zaidi katika filamu anazoziandaa akisema anajaribu kupanua wigo wa waigizaji nchini

Dar es Salaam. Anaigiza, anawaachia nafasi wengine akiwa nyuma ya kamera, anachekesha anapotakiwa kufanya hivyo, ni mnene wa mwili lakini mwongozaji wa filamu akimwamuru kukimbia hana budi kufanya hivyo.
Huyu si mwingine ni Jackob Steven maarufu JB, mmiliki wa kampuni ya utayarishaji filamu iitwayo Jerusalem.
Mwanzoni mwa mwaka huu, aliahidi kutayarisha kazi ya kufungia mwaka ambayo ingetayarishwa katika mikoa kadhaa nchini na kwa bahati, amelikamilisha hilo.
Akizungumzia ahadi yake hiyo mwigizaji huyo mkongwe alisema tayari ameshaitimiza kwa kutayarisha filamu iliyohusisha mikoa minne na Zanzibar akishirikiana na wasanii wa ndani na nje ya nchi.
Aliitaja miji ambayo amefanyia filamu hiyo mpya aliyoipa jina la ‘Mzee wa Swaga’, kuwa ni Visiwani Unguja, Mwanza, Arusha, Dodoma na Dar es Salaam.
Alisema katika kuhakikisha filamu hiyo aliyoiandaa kama zawadi ya kufungia mwaka kwa Watanzania inakuwa bora, aliwashirikisha waigizaji mahiri akiwamo mwigizaji bora wa Zambia Keith Kabwita, mwigizaji bora wa Zanzibar, Kheri Chimbeni, mkongwe Misayo Ndumbagwe maarufu Thea, Wastara Juma na Welu Sengo.
Alieleza kuwa lengo la kukusanya vipaji hivyo na kuzunguka navyo katika mikoa yote hiyo ni kuhakikisha wanapata fursa ya kuona rasilimali zilizopo nchini, pamoja na kujifunza namna ya kutafuta fursa kupitia tasnia hiyo ya filamu.
“Mwongozo wa filamu hiyo ambayo naamini mashabiki wakiiona wataniona nikiwa katika mtazamo mwingine kabisa, ulikuwa unanilazimu kuhama kutoka mkoa mmoja hadi mwingine na nikifika katika mkoa husika natakiwa kukutana na mwenyeji wangu ambaye naye anaingia moja kwa moja katika filamu,” alisema JB.
 Alieleza kuwa ana furaha kubwa kukamilisha zawadi hiyo ya Watanzania na kutimiza ahadi aliyowapa mashabiki wake kuwa, ipo siku atakutanisha waigizaji wa baadhi ya mikoa na kubadilishana uzoefu.
“Unaona mchanganyiko huo, kaa mkao wa kula filamu ni kwa ajili ya mashabiki wangu na mapema mwezi ujao itakuwa hewani,” alisema JB.
Mwigizaji huyo mahiri anayefanya vizuri zaidi akisimama katika filamu na King Majuto, aliitaja sababu inayomfanya awaachie waigizaji chipukizi kufanya kazi badala ya kung’ang’ania kuigiza katika kila filamu anayotayarisha, kuwa ni kujaribu kupanua wigo wa waigizaji nchini.
Alisema kabla yao kulikuwa na kina mzee Kipara, Pwagu na Pwaguzi, Mama Ambiliki, Mzee Jongo, Bi Nyakomba, lakini kwa sababu waliwapa nafasi vijana, hata walipokaa pembeni kwa sababu moja au nyingine, walimudu kuendeleza walipoachia.
Chanzo:Mwananchi

Hakuna maoni: