promotion

Jumanne, 11 Novemba 2014

Mama aibiwa mtoto wake wa miezi miwili baada ya kunyweshwa dawa ya usingizi

Kamanda wa Polisi mkoani Geita, Joseph Konyo


Mtoto mwenye umri wa miezi miwili, ameibiwa baada ya mama yake kudaiwa kunyweshwa dawa za asili na mganga wa kienyeji katika kijiji cha Katoro wilayani Geita.

Kamanda wa Polisi mkoani Geita, Joseph Konyo, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwaonya wazazi kujihami na waganga wa kienyeji wenye dhamira za kuwafanyia ulaghai.

“Upelelezi unaendelea huku mganga wa kienyeji aliyefahamika kwa jina moja la Peranya pamoja na Semeni Thomas, wakisakwa baada ya kutoroka kufutia tukio hilo,’’ alisema Kamanda Konyo.

Kamanda Konyo alimtaja mama aliyeibiwa mtoto huyo kuwa ni Cecilia Twimaniye (20), mkazi wa kijiji cha Kaduda na mtoto aliyeibiwa ni Jackson Shija.
Awali, Mtendaji wa kata ya Katoro, Alloyce Kamuli, alisema baada ya ofisi yake kuarifiwa tukio hilo, waliripoti Kituo cha Polisi Katoro na kufunguliwa jalada la wizi wa mtoto KTR/RB/1194/2014 Oktoba 27.

Akizungumza na NIPASHE, mama wa mtoto huyo, Cecilia, alisema siku ya tukio alishawishiwa na mtuhumiwa Thomas ampeleke kwa mganga ili akatibiwe bawapopo, lakini walipofika huko alipewa dawa ya kuoga na kunywa na kumsababishia kupoteza kumbukumbu na kuhisi kuchanganyikiwa.

“Nikiwa katika hali hiyo, Thomas alimbeba mtoto na kunitaka anisindikize nyumbani, lakini kabla hatujafika alitoroka na mtoto baada ya kudai anaingia chooni,” alisema Cecilia.

Hili ni tukio la pili la kuibiwa kwa mtoto katika mazingira ya kitatanishi.

Mwaka juzi, kichanga kingine kiliibiwa wakati wa ibada ya mahubiri katika moja ya makanisa kijijini hapo na mpaka sasa hakijapatikana.

Hakuna maoni: