Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Anna Makinda. |
Bunge la Jamhuri ya Muungano linatarajia kuwaka moto leo litakapoanza vikao vyake ambapo mambo mbalimbali yatajadiliwa.Tayari Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, imesema imepokea Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali wa mwaka 2014, unaopendekeza kuzifanyia marekebisho sheria 33, ambapo pia utawasilishwa katika vikao vyake.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, William Ngeleja alisema hivi karibuni jijini Dar kuwa kati ya sheria hizo 33, imo Sheria ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, Sura Namba 370 inayopendekeza kuongeza wigo wa wanafunzi kupatiwa mikopo ya elimu ya juu.
“Ikumbukwe haya bado ni mapendekezo, lakini moja ya mapendelezo yaliyopo kwenye sheria hii ya mikopo ni pamoja na kuwajumuisha wanafunzi waliomaliza chuo cha sheria wanaokwenda shule ya sheria nao kupatiwa mikopo,” alisema Ngeleja.
Alisema pia muswada huo umejumuisha Sheria ya Mbegu sura namba 308 iliyoongezewa makali kwa kampuni ambazo zinasambaza mbegu kwa wakulima kuhakikisha zinasambaza mbegu zenye viwango vinginevyo adhabu kali iliyoongezwa ya faini ya kuanzia Shilingi milioni 100 hadi 500 itawakabili.
Alisema kwa sasa takriban Watanzania asilimia 75 wanaishi vijijini na wanajishughulisha na kilimo lakini wengi wao wamejikuta wakipata matatizo katika eneo la mbegu kutokana na sheria zilizopo kushindwa kuzibana kampuni zinazozalisha mbegu.
Sheria nyingine zilizopo kwenye muswada huo ni pamoja na Sheria ya Huduma za Maji na Usafi wa mazingira sura namba 272 na Sheria ya Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi sura namba 179.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni