promotion

Jumanne, 11 Novemba 2014

Wanawake wapinga Foreplan Kliniki kufungiwa




ZAIDI ya wanawake 200 jijini Dar es Salaam,  wameandamana hadi katika ofisi za Foreplan Kliniki, iliyopo Ilala-Bungoni, kupinga hatua iliyochukuliwa na serikali ya kukifungua kituo hicho mwishoni mwa wiki iliyopita.
Wiki iliyopita Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ilikifunga kituo hicho kutokana na kuonekana kukiuka taratibu za kitabibu zinazopaswa kufuatwa na wataalam wa tiba asili nchini.
Wakizungumza na Tanzania Daima jana, baadhi ya wanawake hao walisema wamelazimika kuonyesha hisia zao na kuitaka serikali kukifungua kituo hicho ambacho kimekuwa mkombozi kwao hasa katika matatizo yao ya uzazi.
Mmoja wa wanawake hao, Theresia Mgombela, alisema alisumbuliwa na tatizo la kutokana damu bila kukoma na alizunguka hospitali zote za jijini bila kupata nafuu, lakini baada ya kufika kituoni hapo alipata tiba iliyotibu maradhi yake.
“Hii serikali haina huruma…huyu mtu anasaidia wanawake wengi sana na badala ya kushirikiana naye wanaamua kumdidimiza hii sio haki hata kidogo,” alisema.
Alisema serikali hadi sasa imeshindwa kumchukulia hatua Mchungaji Ambilikile Mwasapile ambaye alishiriki kwa asilimia kubwa kuwaumiza watu wengi na badala yake ilimjengea hadi barabara katika eneo hilo.
Naye Hasimu Kiluke, alisema serikali inachopaswa kukifanya ni kushirikiana na mtaalam huyo, ili kuweza kufanikisha tiba bora na sio kumkandamiza kama ilivyofanyika hivi sasa.
Mmiliki wa kituo hicho, Dk Juma Mwaka, alisema serikali ilikifunga kituo hicho bila kutoa taarifa wala kumfanyia ukaguzi kama inavyotakiwa.
“Kuna watu zaidi ya 40 nimewaajiri, wapo wagonjwa wanaofika kila siku kwa ajili ya kuchukua dawa sasa kutokana na kufungwa kwa kituo wanaweza kupata madhara zaidi,” alisema.
Dk Mwaka alisema yeye kama mtaalam wa tiba asili hafanyi matangazo, bali anatoa elimu kuhusiana na maradhi mbalimbali, ili kuweza kuwasaidia makundi mbalimbali yanayokabiliwa na magonjwa ikiwemo yale ya ugumba.


Hakuna maoni: