Jumatatu, 13 Oktoba 2014
Mtumbwi waua watu 10 wakitoka harusini
Watu 10 wamefariki dunia na wengine 11 kujeruhiwa wakati wakitoka kusherehekea harusi baada ya mitumbwi miwili waliyokuwa wanasafiria kuzama katika Ziwa Tanganyika, eneo la kijiji cha Kalalangabo, mkoani Kigoma.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Dk. Leonard Subi, amethibitisha kupokea maiti tatu na majeruhi 11 na kwamba ajali hiyo ilitokea juzi mchana na maiti tatu ziliopolewa saa moja usiku siku hiyo.
Alisema maiti tatu hazijatambuliwa majina yao ambazo ni za watoto wawili na mwanamke mmoja zilizopatikana juzi jioni na nyingine tatu zilipatikana jana na kutambuliwa na wananchi wameombwa kujitokeza kutambua ndugu zao.
Mkuu wa mkoa wa Kigoma, Issa Machibya, aliamuru kila mwili unaoopolewa kwenda kuzikwa haraka badala ya kupelekwa hospitali na alipotakiwa kuzungumzia tukio hilo kama Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa alikataa na kusema msemaji ni Kamanda wa Polisi wa mkoa.
Maiti zilizopatikana jana ni za Masood Ally (75), Fitina Issa (45), Rehema Kassim (17), Mahamudu Ulimwengu (6), Hawa Gamba (8), Jacob Rashid (1) na Hawa Gwampote (70).
Inadaiwa mitumbwi hiyo ilikuwa na watu zaidi ya 70 na hadi sasa walioopolewa na kuokolewa ni 21 pekee.
Dk. Subi alisema waliofariki ni watoto wawili wa kike na mama mmoja ambao hawajatambulika majina yao na miili yao imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti Hospitali ya Mkoa Maweni.
Aliwataja majeruhi 11 waliolazwa katika wodi namba tano ya Hospitali ya Mkoa Maweni kuwa ni Zaujath Anzuruni (35), Mariam Hamis (30), Zabibu Issa (20), Amina Ramadhani (48), Achi Kashinde (20), Mariam Madua (24), Hawa Mahamoud (40), Yape Said (35), Sijapata Masudi (45) na Hasma Dunia (35) na hali zao zinaendelea vizuri.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Kigoma, Jaffari Mohamed, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa wanaendelea na upelelezi ili kuwabaini watu ambao hawajapatikana na kuopoa miili iliyosalia.
Dk. Suli alizitaka mamlaka husika na watu wote wazingatie sheria, wasizidishe idadi ya abiria na vyombo vya usafiri vikaguliwe na kuaangalia hali ya hewa kama ni mbaya waahirishe safari.
“Jambo la msingi na muhimu ni suala la mawasiliano kwa sababu hata ikitokea ajali yoyote kuwa na mawasiliano wanapotoka mahali fulani waache mawasiliano na wanapozidi kwenda mbali mawasiliano yawapo kama kuna tatizo liweze kujulikana mapema na msaada uweze kutolewa kwa wakati,” alisema.
Mmoja wa majeruhi wa ajali hiyo, Amina Ramadhani (48), akizungumza na NIPASHE katika wodi namba tano Hospitali ya Mkoa ya Maweni, alisema walikuwa wakitokea kwenye harusi ya mwanaye, Ramadhani Hamisi, ambaye alimemuoa Mariam Madua, katika kijiji cha Mwandiga kuelekea kijiji cha Kigalye.
Amina alisema walimaliza sherehe hiyo majira ya saa 7 mchana na kupanda mtubwi katika kijiji cha Kalalangabo kuelekea kijiji cha Kigalye.
“Baada ya kuanza safari tukiwa katikati ya ziwa palizuka mawimbi makubwa, tukiwa ndani ya mitumbwi aina ya vipe iliyounganishwa kwa miti kwa ajili ya kukabiliana na mawimbi ambayo ilikatika na kusababisha mitumbwi hiyo kuzama,” alisema.
Amina alisema idadi ya watu waliokuwa ndani ya mitumbwi hiyo haijulikani na kwamba walikuwa wengi sana wakimsindikiza bibi harusi katika kijiji cha Kigalye.
“Baada ya mitumbwi kuzama watu walihangaika sana wenye uwezo wakujiokoa kwa kuogelea, bahati nzuri ikaja mitumbwi kutoka kijiji cha Kigalye na kuokoa wale waliyokuwa wakiogelea na wengine wakiwa wamezama,” alieleza na kuongeza:
“Naiomba serikali itutengenezee Pantoni kwa ajili ya wakazi wa vijiji vya mwambao mwa Ziwa Tanganyika, tunakufa kila wakati kwa kuzama maji na usafiri wetu ni mitumbwi hakuna barabara, serikali ituletee usafiri kama walivyopelekewa watu wa mikoa mingine, sisi tangu nchi yetu ipate Uhuru hatuna usafiri wa kuaminika, tunatumia mitumbwi ya kuvulia samaki ndiyo inayosafirisha abiria.”
Dada wa bibi harusi, Hasma Dunia (35), alisema walipanda mitumbwi miwili ambayo ilikuwa inatumia mashine moja baada ya kusafiri kilomita tano mashine ilizimika wakatengeneza na walipoiwasha iliwaka wakaendelea na safari ya kwenda Kigalye.
Alisema walipofika katikati ya maji katika Ziwa Tanganyika kwa sababu mitubwi ilikuwa ni miwili imeshikana kwa kutumia miti, mti mmoja wa mbele ulikatika kutokana na mawimbi makubwa baada ya muda mfupi mti wa nyuma nao ukakatika ikabidi mitumbwi yote miwili ikakutana na kuzama kwenye maji.
“Baada ya kuzama ilitufunika, watu waliyokuwa nchi kavu waliona na kuja kutuokoa na kutupeleka Hospitali ya Mkoa ya Maweni,” alisema.
“Tuliokuwa tumepanda mitumbwi kumsindikiza bibi harusi tulikuwa watu wengi sana na tuliyookolewa ni wachache, bibi yangu na mdogo wangu bado maiti zao hazijaokolewa, tunasubiri kesho (jana) zitakapoinuka, kwa leo (juzi) nimeona maiti tatu watoto wawili akiwamo mtoto wa dada yangu na mama mmoja,” alieleza.
Alisema bibi harusi Mariamu Madua na bwana harusi Ramadhani Hamis waliokolewa, lakini bibi harusi amelazwa Maweni kwa matibabu zaidi.
Zoezi la kuwatafuta watu wengine waliozama katika Ziwa Tanganyika lilikuwa linaendelea jana jioni hadi tunakwenda mitamboni, huku zikiwapo taarifa kuwa mitumbwi hiyo ilikuwa imebeba takribani watu 70.
Zoezi hilo linafanywa na wavuvi kwa kushirikiana na askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ)
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni