promotion

Ijumaa, 31 Oktoba 2014

MAAFISA WALIOBAINISHA UFISADI WA BILIONI 40 WATISHIWA KIFO




SAKATA la ubadhirifu wa bilioni 40 katika halmashauri ya jiji la Mwanza limechukua sura mpya baada ya maofisa wa ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) walioibua sakata hilo kudai kutishiwa maisha.

Hayo yalibainishwa jana na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa, Rajab Mohammed Mbarouk wakati wa kikao cha majumuisho ya ziara yao mkoani hapa ambacho hakikuendelea kufanyika kutokana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Hawa Ghasia au mwakilishi wake kutofika katika majumuisho hayo.

“Tumepokea taarifa ya kutishiwa amani kwa baadhi ya wakaguzi, tunasema ofisi ya CAG ipo kisheria na kikatiba na wanafanya kazi kwa kufuata sheria na Katiba,” alisema Mbarouk na kuongeza kuwa, kama wabunge watahakikisha wanatunga sheria na kuzisimamia na kwamba wakaguzi waendelee na kazi yao bila ya hofu.

Mbarouk alimpongeza Mkaguzi Mkazi pamoja na timu yake kwa kuwa na uzalendo wa kitanzania wa kutaka kuokoa uchumi wa Mwanza ambao kwa asilimia 90 unahujumiwa.

Alisema uchumi wa Mwanza unatokana na mapato na miradi ya maendeleo ambapo maeneo hayo yakifanyiwa kazi isiyoridhisha CAG anawajibu wa kutoa taarifa.

Alisema kama Mkaguzi Mkazi ameweza kuwasilisha taarifa yake kwa Bunge pamoja na kwa Rais. Awali, Mjumbe wa kamati hiyo, Kange Lugora alisema kamati hiyo iliishauri wizara husika kushirikiana nao pamoja tangu mwanzo wa ziara yao katika majumuisho ya kamati hiyo ili kubaini yanayotendeka katika miradi ya maendeleo.

“Kitendo cha wizara kutoshiriki katika majumuisho ya kamati hii ni kuendelea kuhalalisha ubadhirifu unaoendelea kwenye halmashauri, tunaonyeshwa miradi hewa na serikali ngazi ya wizara ilipaswa wajionee wenyewe,” alisema.

Aliongeza kuwa, ili waweze kuwatendea haki Watanzania na wana Mwanza, kamati iliagiza kuwa hawawezi kuendelea na mahesabu ya halmashauri ya jiji la Mwanza hadi wizara itakapomrudisha Mkurugenzi wa zamani wa jiji hilo, Wilson Kabwe ambaye kwa sasa amehamishiwa Dar es Salaam.

Alisema kwamba wizara haijafanya jitihada za kumrejesha mkurugenzi huyo na kudai kuwa mazingira hayo yanawafanya washindwe kuwatendea haki Watanzania.

Alisema ili kamati ilinde heshima yake na kwa mazingira hayo hawataweza kufanya majumuisho kwani kwa kufanya hivyo ni kuwasaliti Watanzania.


Hakuna maoni: