RAIS Jakaya Kikwete ameongoza maelfu ya wakazi wa mji wa Moshi na mikoa ya jirani katika mazishi ya Meja Jenerali mstaafu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Muhidin Mfaume Kimario (76), yaliyofanyika makaburi ya Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro.
Meja Jenerali Kimario, aliyewahi kushika nyadhifa mbalimbali ndani ya Jeshi na serikalini katika vipindi tofauti, alifariki dunia Oktoba 6 mwaka huu, katika hospitali ya Apollo nchini India, alikokuwa akipatiwa matibabu kwa muda mrefu.
Utaratibu wa mazishi ulianza majira ya saa 4 asubuhi nyumbani kwa marehemu mtaa wa Swahili, ambako waombolezaji walipata nafasi ya kutoa heshima za mwisho pamoja na dua maalumu ya kumuombea marehemu iliyosomwa na Mwenyekiti wa Bakwata Moshi, Hussein Chifupa.
Baada ya taratibu hizo za nyumbani, jeneza lilibebwa hadi msikiti wa Riadha, ambako ilifanyika swala ya kumuombea marehemu iliyoongozwa na Imamu wa Msikiti huo, Khalifa Abdi Salimu kabla ya safari ya kuelekea kwenye makaburi ya Manispaa.
Jeshi la Wananchi lilipokea Jeneza la Marehemu mara bada ya kufikishwa katika eneo la makaburi, ambako taratibu za kijeshi zilianza kwa Gwaride maalumu la mazishi, ambako mizinga 11 ilipigwa ikiwa ni sehemu ya kutoa heshima ya kijeshi kwa Marehemu.
Mara baada ya kumalizika kwa taratibu hizo, Mkuu wa Batalioni ya Kaskazini, Meja Jenerali Ezekiel Kyunga, akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya Mkuu wa Majeshi nchini (CDF), Jenerali Davis Mwamunyange, alimtaja marehemu Kimario kama mbuyu ambao umeanguka wakati mchango wake bado unahitajika.
Akitoa shukurani kwa niaba ya familia, Mtoto wa Marehemu, Mfaume Kimario, alimshukuru Rais Kikwete kwa kufika kuwafariji pamoja na kuwaunga mkono katika kipindi hicho kigumu.
Wakati huo huo, Rais Kikwete jana aliungana na waombolezaji kutoa heshima za mwisho na kuaga mwili wa Katibu Mkuu wa Kwanza Mwafrika wa Chama cha Mabunge ya Jumuia ya Madola (CPA), Dk. William Shija, ambaye pia alipata kuwa Waziri Mwandamizi wa Serikali, katika shughuli iliyofanyika kwenye viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam.
Dk. Shija ambaye alifariki dunia Oktoba 4 kwenye Hospitali ya Charing Cross mjini London, Uingereza ambako alikuwa anapata matibabu ya ugonjwa wa Saratani, atazikwa leo kijijini kwao, Nyalukomba, Sengerema, Mwanza.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni