JESHI la polisi nchini limethibitisha kuwa kitu kilichokuwa kinadaiwa kuwa ni bomu lililorushwa mjini Songea mkoani Ruvum Septemba 16 mwaka huu majira ya saa 1.25 usiku katika eneo la Misufini na kuwajeruhi askari polisi watatu kati ya wanne waliokuwa doria kuwa ni bomu la kutupwa kwa mkono lililotengenezwa kienyeji.
Akitoa taarifa ya uchunguzi wa tukio hilo kwa waandishi wa habari mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai kamishina wa polisi Isaya Mngulu amesema bomu hilo lilirushwa na watu wasiojulikana na kuwajeruhi askari polisi watatu waliokuwa doria siku hiyo wa kituo kikuu cha polisi cha mjini Songea ambao ni G.5515 PC John,G7351 PC Ramadhan na WP 10399 Felista ambao baaada ya kujeruhi kwa bomu hilo walikimbizwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Ruvuma iliyopo mjini Songea kwa matibabu.
Amesema askari PC John aliyepata majeraha kiasi alipatiwa matibabu siku hiyo na kuruhusiwa huku askari wawili PC Ramadhan na WP Felista wakiendelea kupatiwa matibabu hospitalini hapo na hali zao zinaendelea vizuri.
Aidha amesema jeshi la polisi makao makuu kwa kushirikiana na jeshi la polisi mkoani Ruvuma na vyombo mbali mbali vya ulinzi na usalama vinaendelea na uchunguzi zaidi ikiwa ni pamoja na kutafuta taarifa za waliohusika na tukio hilo ambalo mpaka sasa hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana nalo.
Amesema jeshi la polisi linaamini kuwa wahusika waliofanya tukio hilo ni sehemu ya jamii inayoishi mjini Songea au yenye mahusiano na wenyeji wa Songea na mtu aliyetengeneza bomu hilo lazima kuna mtu au watu walioshuhudia au wanaomjua kwa maana kwamba hakuwa pekee yake na ni imani ya jeshi la polisi kuwa kuna baadhi ya wananchi wanaweza kuwa wanawafahamu wahusika wa tukio hilo, hivyo wasisite kushirikiana na jeshi la polisi kuwafichua ili kuendeleza ushirikiano mwema na jeshi la polisi kwa ulinzi.
Katika hatua nyingine mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai, Kamishina wa polisi Isaya Mngulu ametoa wito kwa wananchi kuendeleza ushirikiano kwa vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na timu ya upelelezi kutoka makao makuu ya jeshi la polisi kwa ajili ya kuwapata wahusika wa tukio hilo ambalo limetokea kwa mara ya kwanza mkoani Ruvuma na lisipofanyiwa kazi ipasavyo linaweza kutoa mwanya kwa wahalifu wa aina hiyo kuendeleza uhalifu huo kwa wananchi pamoja na jeshi la polisi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni