Jumatatu, 25 Agosti 2014
Chadema waongeza kurudisha fomu
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesitisha muda wa mwisho wa kuchukua na kurudisha fomu za kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama hicho katika uchaguzi wake mkuu wa mwaka huu.
Mkurugenzi wa Oganaizesheni, Mafunzo na Usimamizi wa Kanda wa Chadema, Singo Kigaila, alisema chama kimeona vyema kusogeza muda wa kuchukua na kurejesha fomu hizo kutokana na maombi mengi ya wafuasi wake kutoka wilayani na mikoani.
Kwa mujibu wa Kigaila, kabla ya mabadiliko, muda wa mwisho wa kurudisha fomu katika uchaguzi huo wa kitaifa ulikuwa leo, lakini baada ya maombi hayo, waliona vyema kusogeza siku saba mbele kuanzia jana hadi Agosti 30, mwaka huu.
“Tumekubaliana kuongeza mbele muda wa siku saba zaidi ili kuepusha malalamiko. Sasa tarehe ya mwisho ya kurudisha fomu itakuwa Agosti 30 jioni mwaka huu,” alisema.
Alisema walianza ngazi ya msingi (vitongoji), matawi, kata, jimbo, wilaya na sasa wapo ngazi ya mikoa na kwamba hadi jana walishakamilisha idadi ya mikoa 19 kati ya 32 ya kichama Tanzania Bara na Zanzibar.
Aliongeza kuwa, mkutano mkuu wa chama hicho utafanyika Septemba 14 mwaka huu katika ukumbi wa Mlimani City kwa ajili ya uchaguzi wa viongozi ndani ya chama hicho wakiwamo Mwenyekiti Taifa kwa upande wa Tanzania Bara na Makamu Mwenyekiti kutoka Zanzibar.
Alisema kwa sasa wameshakamilisha mchakato wa uchaguzi huo kwa asilimia 93 kwa maana ya kwamba kati ya majimbo 239 ya kichama, wameshakamilisha majimbo 223.
Baadhi ya nafasi zinazogombewa ndani ya chama hicho ni Mwenyekiti wa Taifa kutoka Tanzania Bara, Makamu Mwenyekiti kutoka Zanzibar,
wenyeviti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha) na wajumbe wa Kamati Kuu ya chama.
Kuhusu wazee wa chama hicho kutoka mkoani Kigoma, kwenda kumchukulia fomu Mwenyekiti waTaifa wa Chadema ili aweze kuwania tena nafasi hiyo, alisema, maamuzi ya kugombea anayo mgombea mwenyewe.
Wengine waliochukua fomu ni pamoja na Upendo Peneza (26) kutoka Mwanza, anawania nafasi ya Mwenyekiti Taifa ndani ya Bavicha, Julius Mruta wa Dar es Salaam, Alex Mushi , Efatha Nanyoro ambaye ni Diwani wa Arusha, pamoja na Lilian Wassira anayewania nafasi ya Mwenyekiti Taifa, Bawacha.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni