Mhe. Mama Salma Kikwete, Mlezi wa MEWATA;
Mhe. Kebwe Steven Kebwe (Mb.), Naibu Waziri wa Afya
na Ustawi wa Jamii;
Mhe Fatma Mwasa, Mkuu wa Mkoa wa Tabora;
Wakuu wa Wilaya – Tabora, Nzega na Urambo;
Wabunge Wote wa Mkoa wa Tabora Mliopo;
Dkt. Serafina Mkuwa, Mwenyekiti wa MEWATA;
Wawakilishi wa Washirika Wetu wa Maendeleo;
Dkt. Joseph Komwihangiro, Mwakilishi wa Marie
Stopes;
Madaktari Wote wa MEWATA na Watumishi wa Sekta ya
Afya;
Mwakilishi wa Shirika la Marie Stopes na
Wawakilishi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Waliopo;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Shukrani na Pongezi
Niruhusuni nianze kwa kuwashukuru Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii,
Dkt. Seif Rashid (aliyewakilishwa hapa leo na Naibu Waziri Mhe.Dkt. Stephen
Kebwe) na Mwenyekiti wa Chama cha Madakatari Wanawake Tanzania (MEWATA), Dkt.
Sarafina Mkuwa kwa kunialika kuja kuzindua huduma za uchunguzi wa saratani ya mlango
wa kizazi na saratani ya matiti Mkoani Tabora.
Nawapongeza nyote kwa maandalizi mazuri kwani ni ukweli usiopingika kuwa
shughuli hii imefana sana. Aidha, nawashukuru
wenyeji wetu wa Mkoa wa Tabora wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa, Mheshimiwa Fatma
Mwasa, kwa mapokezi mazuri mliyonipatia mimi, mke wangu na wageni wenzetu.
Sikutegemea kupata mapokezi tofauti na haya hapa Tabora, kwani upendo wenu
kwangu na ukarimu wenu tunaujua na unasifika na wengi.
Madhumuni ya Ziara
Ndugu Wananchi;
Nimekubali kuja kujumuika nanyi katika uzinduzi huu, siku ya leo, ili
kuongeza sauti yangu na uzito kuhusu shughuli hii muhimu na adhimu inayofanywa
na Madaktari Wanawake hapa nchini. Ni
ukweli ulio wazi kuwa MEWATA imesaidia kuokoa maisha ya akinamama wengi nchini
ambao, vinginevyo, wangepoteza uhai kwa saratani hizi mbili zinazowapata
wanawake. Hatuna budi kuvunja ukimya na
kuungana na Madaktari Wanawake kuzungumzia maradhi haya na kuelimishana ili
wananchi, wadau na Serikali kwa umoja wetu au mmoja mmoja, tuchukue hatua stahiki
za kukabiliana na maradhi haya.
Aidha, ni nafasi nzuri ya kutoa pongezi zangu kwa wanachama wa MEWATA
kwa kazi kubwa na nzuri waifanyayo na mafanikio yaliyopatikana. Sijui hali ya maradhi haya ingekuwaje hapa
nchini kama Madaktari Wanawake wasingeamua kufanya kazi hii njema
wanayoifanya. Kwa niaba ya wanawake na
wanaume wote wa Tanzania tafadhali pokeeni pongezi zetu za dhati. Endeleeni kufanya kazi hii njema na Mwenyezi
Mungu atawalipa kwa wema wenu na mioyo yenu ya huruma. Nawaahidi kuendelea kuwaunga mkono kwa hali
na mali na kwa kadri ya uwezo utakavyoniruhusu.
Nimefurahi sana kwamba ndugu zetu wa MEWATA wameweza kufika hapa Tabora
siku ya leo. Mtakumbuka kuwa nilipokuja
kwenye Sherehe za Siku ya Wanawake Duniani tarehe 8 Machi, 2010, niliahidi
kwamba nitawaomba MEWATA waje kufanya uchunguzi wa saratani za mlango wa kizazi
na matiti kwa akinamama. Hayawi hayawi
leo yamekuwa. Nawashukuru sana viongozi
na wanachama wa MEWATA kwa kuja kwenu.
Mmenitoa kimasomaso. Wahenga walisema: “Ada ya Mja kunena,
muungwana na vitendo”. Ndugu zangu wa
Tabora ahadi imetimia, kazi kwenu. Jitokezeni
kwa wingi kupima muokoe maisha yenu.
Hali ya Magonjwa ya
Saratani ya Wanawake Nchini
Ndugu Wananchi,
Tanzania inatambulika
kuwa ni moja ya nchi zenye kiwango kikubwa cha maradhi ya saratani ya mlango wa
kizazi hapa Afrika ya Mashariki. Inakadiriwa
kuwa takriban wanawake 56 katika
kila wanawake 100,000 hupata saratani
hii. Inakadiriwa pia kuwa zaidi ya watu 35,000
wanapata saratani hii kila mwaka na zaidi ya watu 27,000 hupoteza maisha. Mwaka 2010 peke yake, wanawake wapatao 6,000 waligundulika kuwa na saratani ya
mlango wa kizazi na wanawake 4,000
kati yao walifariki dunia.
Wataalamu wanatuambia
kuwa, saratani hii huwapata wanawake wa umri wa miaka 30 na 50. Aidha, wanawake wanaoishi na virusi vya
UKIMWI wako katika hatari zaidi ya kupata ugonjwa huo kwa asilimia 50. Pamoja na
tatizo hili, bado tunayo changamoto ya saratani ya matiti ambayo ni ya pili kwa
kusababisha vifo vya wanawake wengi nchini.
Hivyo basi, hapa nchini wanawake wako kwenye hatari kubwa ya kufa kwa saratani
kuliko wanaume kwa sababu saratani nyinginezo, hazibagui ukiacha ile ya
tezidume inayowapata wanaume pekee.
Hatua za Tahadhari za Kuzingatiwa
Bahati nzuri, saratani ya
mlango wa kizazi na saratani ya matiti zinaweza kutibika ikiwa zitagunduliwa mapema. Njia pekee ya kuweza kugundua mapema ni
kupima mara kwa mara. Wataalamu
wanashauri kuwa ni vyema wanawake wenye umri wa kati ya miaka 30 na 50
wakachunguza afya zao walau mara moja katika kila miaka mitatu. Na, kwa wanawake wanaoishi na virusi vya
UKIMWI wanashauriwa kuchunguzwa walau mara moja kwa mwaka.
Bahati mbaya sana, uzoefu
umeonyesha kuwa wanawake wengi hufika hospitali wakati ambapo ugonjwa umeshapea
na kuenea sehemu nyingine za mwili. Wanakwenda
hospitali wakati maradhi yamefikia hatua isiyoweza kutibika na hivyo kupoteza
maisha. Hivyo basi, kupima na
kugundulika mapema kwa saratani ni hatua muhimu sana ya kuepusha vifo vinavyotokana
na maradhi hayo. Bahati nzuri hivi karibuni kumekuwepo na mwamko na mwitikio mzuri
wa kujitokeza kwa wanawake wengi kupima saratani ya matiti. Haya ni matunda ya kazi nzuri inayofanywa na
MEWATA. Juhudi hizi zinapaswa
kuendelezwa. Zinastahili kuungwa mkono.
Hatua Zinazochukuliwa na Serikali
Ndugu Wananchi;
Serikali imechukua hatua mbalimbali katika kukabiliana na saratani ya mlango
wa kizazi. Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imeanzisha Programu inayoshughulikia
masuala ya Saratani za Uzazi katika Kitengo cha Afya ya Uzazi na Mtoto mwaka
2008. Kupitia programu hii tuna Mpango Mkakati wa Kukinga na Kudhibiti Saratani
ya Mlango wa Kizazi (2011-2016). Mwongozo
wa kutoa huduma umeandaliwa pamoja na miongozo
ya mafunzo kwa watoa huduma na ujumbe wa kuelimisha jamii kupitia njia
mbalimbali. Kupitia programu hii tumeweza kuanzisha vituo zaidi ya 130
vinavyotoa huduma ya uchunguzi wa Saratani ya Mlango wa Kizazi katika Mikoa 17 hapa
nchini. Ukilinganisha na mwaka 2008 tulipokuwa
na vituo vinne tu vilivyokuwa vinatoa huduma hii ya uchunguzi wa Saratani ya Mlango
wa Kizazi na tiba ya mabadiliko ya awali, haya ni maendeleo makubwa.
Ndugu Wananchi,
Kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Serikali imeendelea
kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo MEWATA, Marie Stopes, WAMA na wengineo
kutekeleza mpango wa “Utepe wa Pinki na Utepe Mwekundu” yaani “Pink Ribbon Red Ribbon”. Kupitia program hiyo, kampeni ya uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi na matiti
ilizinduliwa katika mkoa wa Mwanza mwezi Machi mwaka huu katika kuadhimisha Siku
ya Wanawake Duniani.
Kupitia mpango huo, tumekabidhi mashine 16 za kutolea huduma za matibabu
ya mabadiliko ya awali ya saratani ya mlango wa kizazi (Cryotherapy machine) kwa mikoa ya
Mwanza, Mara, Iringa, Njombe na Mbeya. Mipango inaendelea kwa mikoa iliyosalia
pamoja na Tabora kupatiwa mashine hizo kuendeleza juhudi za Serikali kupanua upatikanaji
wa huduma hizi katika mikoa yote nchini.
Lengo letu katika kufanya hivyo ni kutaka kupunguza mzigo mkubwa
unaoielemea Hospitali yetu ya kuu kansa ya Ocean Road. Pia, tunataka kuwapunguzia wanawake adha na
gharama ya kusafiri umbali mrefu hadi Dar es Salaam kwa ajili ya
uchunguzi. Tunatambua umuhimu wa huduma hizi
kuwa karibu zaidi na walipo watu ili ziwafikie
wanawake wote bila kujali hali zao za kipato.
Ndugu Wananchi;
Katika jitihada za kutokomeza maradhi haya, Serikali, kupitia Mpango wa
Taifa wa Chanjo, imeanza kutoa chanjo ya kuzuia Saratani ya mlango wa Kizazi ya
“Human Papilloma Virus (HPV)”. Chanjo
hii hutolewa kwa watoto wa kike wenye umri wa miaka 9. Chanjo hii hukinga wasipate maambukizi ya
virusi ambavyo husababisha Saratani ya Mlango wa Kizazi. Wizara ya Afya tayari imezindua
mpango huo wa utoaji wa chanjo ya HPV kwa wasichana tarehe 29 Aprili, 2014 wakati
wa Maadhimisho ya Wiki ya Chanjo Duniani na mama Salma Kikwete. Mpango huo ulizinduliwa
kwa Halmashauri tano za Hai, Siha, Moshi Vijijini, Moshi Mjini na Rombo za Mkoa
wa Kilimanjaro, kuashiria kuanza kwa utekelezaji wa azma ya kutoa chanjo hii
nchi nzima ifikapo mwaka 2016.
Shukrani kwa Wadau
Ndugu Wananchi;
Napenda kutoa pongezi na shukrani za pekee kwa MEWATA kwa kazi nzuri na
kubwa ya kukuza uelewa wa jamii na kuhamasisha uchunguzi wa saratani
zinazowapata wanawake. Ni dhahiri kwamba
ili jambo hili lifanikiwe lazima liwe na mshika bango wake. Bahati nzuri ndugu zetu wa MEWATA wamejitoa
kimasomaso na wamefanya kazi ya Serikali kuwa rahisi. MEWATA imekuwa inafanya kazi kwa karibu na Serikali
pamoja na wadau wengine katika kuhamasisha jamii kuhusu masuala ya Saratani ya
Matiti na ya Mlango wa Kizazi. Kama
nilivyokwisha kusema awali, juhudi hizo zimewafikia wanawake wengi nchini na
kuokoa maisha yao.
Aidha, napenda kuchukua fursa hii kutambua na kutoa shukrani maalum kwa Shirika
la Marie Stopes na wadau wote ambao wanashirikiana na Serikali katika kupambana
na tatizo hili kubwa la Saratani ya Mlango wa Kizazi. Vilevile, tunawashukuru wale wote wanaotoa
huduma ya afya ya uzazi na mtoto nchini. Napenda kwa mara nyingine tena
kuwahakikishia ushirikiano wa Serikali ya CCM ninayoiongoza kwenu. Ni, dhamira yetu kupunguza na ikiwezekana hata kumaliza kabisa vifo vitokanavyo na Saratani ya Mlango
wa Uzazi na Saratani ya Matiti ambazo kwa kweli zinaweza kuzuilika.
Wito kwa Wananchi
Ndugu Wananchi;
Natoa wito kwa wanawake wa Tabora kujitokeza kwa wingi kufanyiwa
uchunguzi wa saratani hizi na wataalamu
walioko hapa. Napenda kuwatoa hofu kuwa saratani
ya mlango wa kizazi na saratani ya matiti siyo magonjwa ya aibu au ya mkosi au uchawi
au laana na wala siyo magonjwa yasiyotibika.
Magonjwa haya huweza kumpata mwanamke ye yote, awe ameolewa au
hajaolewa, awe amezaa au hajazaa, awe tajiri au maskini. Madhali ni mwanamke anaweza kupata. Sharti lake la kupona ni kugundulika mapema
na kuanza tiba mapema. Kuchelewa
kugundulika na kuchelewa kuanza matibabu ndiko kunakosababisha vifo kutokana na
maradhi haya. Waswahili wana msemo
usemao, mficha maradhi kifo humuumbua.
Hivyo ndugu zangu kina mama nashauri mfanye uchunguzi mapema, ili kama kuna
tatizo muanze tiba mapema.
Napenda kutumia fursa hii, kuwaasa akina baba na walezi nao kusaidia katika
juhudi za kuzuia na kutibu magonjwa haya ya saratani ya wanawake. Mwanamke anayepata magonjwa haya anahitaji
matunzo na upendo siyo masimango na unyanyapaa. Masimango na unyanyapaa
huwafanya wanawake waogope kujitokeza kuchunguza afya zao na kupatiwa tiba kwa
kuogopa kubaguliwa au kuachwa. Magonjwa haya yanatibika. Si kila mwanamke anayepata saratani hufariki
dunia. Kinachotakiwa ni baba na mama kushirikiana
kumpeleka mama kufanyiwa uchunguzi na kupata tiba iwapo atagundulika kuwa na
maradhi. Saratani siyo ugonjwa wa zinaa, hivyo, msiwanyanyapae akina mama bali muwalee
na kuwatunza ili waweze kurejea katika hali zao za kawaida. Akina baba muwe ndiyo nguzo ya mafanikio
katika mapambano dhidi ya saratani.
Na, kwa wanaume wenzangu, tujenge mazoea ya kupima afya zetu hususan
kuhusu saratani ya tezidume (prostate).
Hii ni saratani inayoua wanaume wengi duniani na hapa nchini. Lakini nayo kama zilivyo saratani za matiti
na mlango wa kizazi zinatibika kama zitagundulika mapema. Kila mkienda kupima afya pimeni afya ya
tezidume mjue mustakabali wenu.
Ndugu Wananchi;
Sote tukiungana pamoja tunaweza kutokomeza saratani ya mlango wa kizazi
na saratani ya matiti. Nia ya kutokomeza
maradhi haya tunayo, sababu ya kutokomeza tunayo na uwezo wa kuyatokomeza tunao. Kinachotakiwa ni kuunganisha nguvu zetu
pamoja. Mimi na mke wangu Mama Salma
Kikwete tuko nanyi na tutaendelea kuwa nanyi bega kwa bega katika vita hii sasa
na hata baada ya kuacha Urais mwakani.
Inawezekana, timiza wajibu wako!
Ndugu Wananchi;
Kwa vile niko Tabora ni vyema nikatumia nafasi hii pia, kuyazungumzia
baadhi ya mambo niliyoyazungumzia au kuahidi kufanya safari zilizopita. Kwa upande wa barabara, napenda kuwahakikishia
kuwa barabara kuu zinazoendelea kujengwa hapa Mkoani Tabora tutazimaliza. Subira yavuta heri. Barabara ya Urambo –Kaliua ujenzi utaanza mwaka huu wa fedha na
Chaya – Nyahua, mchakato wa kutafuta fedha unaendelea ili nayo ujenzi wake
uweze kuanza kabla ya mimi kumaliza kipindi changu cha uongozi. Kuhusu kupata maji ya Ziwa Victoria, kwa Igunga, Nzega, Tabora, Urambo na Sikonge hatua
za awali zimeanza na kinachofuatia ni kutafuta fedha kwa ajili ya mradi huo
mkubwa. Tunakusudia kuiomba Serikali ya
India ambayo ndiyo iliyogharamia matayarisho ya mradi. Tuna matumaini ya kufanikiwa. Sote tuzidi kuomba iwe hivyo.
Kwa upande wa tatizo la wakulima wa tumbaku kutokulipwa stahili zao na
vyama vya ushirika nimeelezwa na kulielewa.
Kuna tuhuma za wizi na ubadhilifu.
Nimemuagiza Inspekta Jenerali wa Polisi atume watu wake wa upelelezi wa
makosa ya Jinai waje wafanye uchunguzi ili wahusika wakamatwe na kufikishwa
Mahakamani na kupewa adhabu zinazostahili.
Ameniahidi kuwa keshokutwa Jumatatu watu hao watakuja. Wapeni ushirikiano unaostahili ili tukomeshe uhalifu
na dhuluma zinazofanywa na Maofisa wa Vyama vya Ushirika na taasisi za fedha
kwa muda mrefu sasa.
Baada ya kusema hayo, naomba nitangaze sasa zoezi hili la uchunguzi wa
Saratani ya Mlango wa Kizazi na ya Matiti limefunguliwa rasmi.
Nawashukuruni sana.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni