Jumatano, 14 Mei 2014
Milioni 500/- zatengwa kukabili dengue
Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Kebwe Stephen Kebwe
Serikali imetenga Sh. milioni 500 kwa ajili ya kunyunyiza dawa za kuua mazalia ya mbu kwenye maeneo chepechepe jijini Dar es Salaam, katika jitihada za kukabiliana na ugonjwa wa dengue.
Vile vile, imewaagiza watendaji wa vitongoji kusimamia usafi kwenye maeneo yao.
Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Kebwe Stephen Kebwe, aliyasema hayo wakati alitoa kauli ya serikali bungeni jana kuhusu ugonjwa wa homa ya dengue, baada ya Mbunge wa Kigamboni ( CCM), Dk. Ndugulile Faustine, kutaka taarifa ya serikali kuhusu hatua ilizochukua kudhibiti ugonjwa huo.
Dk. Kebwe alisema Wizara imeandaa mpango wa namna ya kukabiliana na ugonjwa huo na kwamba umeshirikisha sekta mbalimbali na kwamba hadi sasa zaidi ya Sh. milioni 132 zimetumika kwa ajili ya ugonjwa huo na kwamba fedha zaidi zitaendelea kutolewa.
“Wananchi wanashauriwa kutokuwa na hofu kuhusu ugonjwa huu kwani hauambukizwi kwa kumhudumia mgonjwa au kwa kugusa maji maji yanayotoka kwa mgonjwa...tunawashauri wananchi kwenda vituo vya afya haraka pindi waonapo dalili za ugonjwa huo,” alisema.
Alisema sehemu kubwa ya ugonjwa huo inachochewa na mazingira machafu na kwamba mvua kubwa zinazoendelea kunyesha zinachangia kuongezeka kwa mazalia ya mbu na kwamba utupaji, uzoaji na uhifadhi wa taka katika miji nchini hauridhishi hali inayotoa fursa kwa mazalia ya mbu kuongezeka.
Dk. Kebwe alisema hadi sasa hakuna chanjo wala dawa maalum kwa ajili ya kudhibiti au kutibu ugonjwa huo na kwamba njia kubwa ni kumzuia binadamu asiumwe na mbu.
USHAURI
Alisema mbinu shirikishi za kutokomeza mbu lazima zitiliwe mkazo na kwamba njia bora na rahisi ni kutokomeza mazalia yote ya mbu.
Pia, alisema watu wavae nguo zinazofunika mikono na miguu na kutumia dawa zinazofukuza mbu, watoto walale kwenye vyandarua vyenye viatilifu wakati wa mchana.
JINSI YA KUJIKINGA
Alisema njia ya kujikinga ni kufukia madibwi ya maji yaliyotuama au kunyunyuzia viuatilifu vya kuua viluwiluwi vya mbu kwenye madibwi, kuondoa vitu vinavyoweza kuweka mazalio ya mbu kama vifuu vya nazi, makopo, magurudumu ya magari na kufyeka vichaka karibu na makazi.
Nyingine ni kuhakikisha maua yanayopadwa kwenye makopo au ndoo hayaruhusu maji kutuama, kufunika mashimo ya majitaka kwa mfuniko imara na kusafisha grata za paa la nyumba ili kutoruhusu maji kutuama.
HATUA ZILIZOCHUKULIWA
Alisema timu ya taifa ya masafa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwamo halmashauri za Jiji la Dar es Salaam na wadau wa maendeleo wanakutana kila mara baada ya wiki mbili kutathmini mikakati ya kamati ya dharura iliyowekwa.
Nyingine alisema serikali ilitoa tamko kuanzia Machi, mwaka huu, kuendelea kutoa taarifa ya taadhari ya ugonjwa huo kupitia kwa waganga wakuu wa mikoa na wilaya, ikiwa ni pamoja na namna mgonjwa anavyoweza kutambuliwa, mwongozo kwa watumsihi wa afya wa namna ya kuchukua sampuli, vipeperushi vinavyoelezea jinsi ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo.
Pia, kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kupitia redio na runinga na kwamba wizara kwa kushirikiana na halmashauri za jiji wameendelea kutumia maafisa afya wakiwamo wa kata na uongozi wa mitaa kuwaelimisha wananchi namna ya kudhibiti ugonjwa kwa kutumia vipaza sauti.
Dk. Kebwe, alisema hatua nyingine ni kutoa elimu ya afya kwa watumishi wa afya pamoja na madaktari na mafundi sanifu wa maabara namna ya kutambua ugonjwa huo katika hospitali za Muhimbili, Amana, Mwananyamala na Temeke.
HALI ILIVYOKUWA JANA
Hospitali kadhaa jijini Dar es Salaam zimeendelea kupokea wagonjwa kwa mujibu wa taarifa za jana.
MWANANYAMALA
Juzi mgonjwa mmoja aligunduliwa na kutibiwa kisha kuruhusiwa na kufanya idadi ya wagonjwa waliothibitishwa kuugua ugonjwa huo katika hospitali hiyo kuwa 140.
Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dk. Faustinias Ngonyani, alisema jana kuwa wagonjwa wote walitibiwa na kuruhusiwa.
Alisema ugonjwa huo ulipolipuka walipokea wagonjwa 139 na mmoja aliongezeka juzi na idadi ya wagonjwa 140 ambamo alisema kati yao wagonjwa sita ni watumishi wa hospitali hiyo, ambao hali zao zinaendelea vizuri.
AGA KHAN
Hospitali ya Aga Khan imesema kwa wiki moja wamepokea wagonjwa 26, kati yao 17 walitibiwa na kuruhusiwa huku tisa wakiwa wamelazwa.
Muuguzi Mkuu wa hospitali hiyo, Loveluck Mwasha, alisema waliolazwa ni Wachina saba na Watanzania wawili na kuwa hali zao zikiendelea vizuri.
MUHIMBILI
Katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) jana alikuwapo mgonjwa mmoja.
Kwa mujibu wa Afisa Uhusiano Mwandamizi wa MNH, Aminieli Eligaesha, mgonjwa huyo alikuwa amelazwa kwenye kitengo cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi wa karibu (ICU) cha hospitali hiyo na alikuwa anafanyiwa vipimo ili kujua ugonjwa unaomsumbua ingawa dalili za awali zilionyesha kuwa anasumbuliwa na dengue.
TEMEKE
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Temeke, Dk. Amani Malima, alisema idadi ya wagonjwa katika hospitali yake imeongezeka na kufikia 20 na kuwa kati yao wapo watumishi 10 wa wilaya hiyo.
DK. BUBERWA AAGWA KWA MAJONZI
Vilio na simanzi vilitawala jana wakati wakuagwa kwa mwili wa Dk. Gilbert Buberwa (36) katika Hospitali ya Temeke jijini Dar es Salaam ambaye alifariki Jumapili iliyopita kwa ugonjwa wa dengue.
Dk. Buberwa ambaye alikuwa daktari bingwa wa magonjwa ya akili, alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Wafanyakazi wa Hospitali ya Temeke pamoja na madaktari wengine walijikuta wakitokwa na machozi wakati wakiuaga mwili huo, huku wengine wakionekana kuwa na majonzi.
Mwakilishi wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, ambaye ni mtaalamu wa magojwa ya akili, Dk. Ayubu Magimba, alisema serikali imepata pigo kubwa kwa kifo cha Dk. Buberwa kwa kuwa alikuwa akitegemewa kwa kiasi kikubwa.
Alisema wanasikitika kumpoteza mtu ambaye alikuwa ni makini na kwa mkoa wa Dar es Salaam alikuwa akitegemewa sana.
Hata hivyo, Dk. Magimba, alishindwa kuendelea kuzungumza kutokana na kutokwa na machozi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana baada ya kuagwa kwa mwili huo, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Temeke, Dk. Amani Malima, alisema hospitali yake imepata pigo kubwa kwani walikuwa wakimtegemea kila idara.
“Dk. Buberwa alikuwa kichwa, pia alikuwa ni msaidizi wangu licha ya kwamba ni daktari bingwa wa masuala ya akili alikuwa na uwezo wa kuangalia idara zote na hata wodi za wanawake alikuwa akitibu hakuna kilichokuwa kinamshinda, hivyo hata nikiondoka ninakuwa sina wasiwasi kwa kuwa nimeacha jembe langu,” alisema Dk. Malima.
Dk. Malima alisema mwili wa marehemu umepelekwa nyumbani kwake Kinyerezi, jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mazishi yatakayofanyika leo.
Imeandikwa na Salome Kitomari, Dodoma, Beatrice Shayo, Jimmy Mfuru, Leonce Zimbandu, Enles Mbegalo, Samson Fridolin na Elizabeth Zaya, Dar
By mcharoman
Chukua tahadhari dengue ni ugonjwa mbaya sana
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni