promotion

Jumanne, 18 Machi 2014

MKAZI WA MAGO MAKETE AUAWA KWA KUCHOMA KISU NA MUME MWENZIE, KISA WIVU WA KIMAPENZI

























Mkazi wa kijiji cha Mago kata ya Lupalilo wilayani Makete mkoa wa Njombe Bw. Frenk Sanga (35) ameuawa kikatili kwa kuchomwa kisu kifuani upande wa kushoto ambao ndipo moyo ulipo kwa kile kinachodaiwa kuwa ni wivu wa kimapenzi

Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia Machi 17 mwaka huu majira ya saa 7 usiku, ambapo mtuhumiwa aitwaye Yohana Sanga alimchoma kisu kifuani baada ya kumfumania akiwa na mpenzi wake(hawara) aliyetambulika kwa jina la Matilda Sanga ambaye pia ni mkazi wa kijiji hicho cha Mago

Imeelezwa kuwa siku ya tukio marehemu ambaye alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na Bi. Matilda, waliongozana usiku hadi nyumbani kwa mwanamke huyo kwa ajili ya kulala pamoja, na ndipo mtuhumiwa ambaye ni Yohana, ambaye inadaiwa alikuwa akifuatilia nyendo zao aliwavamia nyumbani kwa mwanamke huyo na kumchoma kisu kifuani marehemu hadi akapoteza maisha

Baada ya mtuhumiwa kutenda mauaji hayo katika nyumba ya huyo hawara yake alichomoa kisu hicho na kumshikisha marehemu mkononi, kwa lengo la kupoteza ushaidi ili ionekane kuwa alijiua mwenyewe

Akizungumzia tukio hilo Afisa upelelezi wa polisi wilaya ya Makete ambaye pia ni Kaimu OCD wilaya ya Makete, Mrakibu wa polisi Gosbert Komba amesema wao kama jeshi la polisi walipewa taarifa na Bw. Emannuel Sanga (25) ambaye aligundua kuuawa kwa marehemu Frenk na wao kama polisi walifuka eneo la tukio na kuthibitisha mauaji hayo

Bw. Komba amesema mtuhumiwa wa mauaji hayo amekimbia mara baada ya tukio na jeshi hilo linamtafuta na kutoa wito kwa wananchi kwa kuwa mtuhumiwa anafahamika watoe taarifa polisi endapo watamuona ili atiwe mbaroni

Amesema kwa sasa wanamshikilia mwanamke huyo kwa mahojiano zaidi kuhusiana na tukio hilo, na katika mahojiano na jeshi hilo mwanamke huyo amesema alishaachana na Yohana ambaye ni mtuhumiwa aliyetenda mauaji hayo na kwa sasa mapenzi yake yalikuwa kwa marehemu Frenk

"Kwa kawaida huyu mwanamke aligonganisha magari (aligonganisha wapenzi), na sisi kama polisi tunatoa wito kwa hawa dada zetu au wanawake, kuwa na mpenzi mmoja, lakini pia watu wasijichukulie sheria mkononi" alisema Komba

Wakizungumza baada ya kumzika marehemu baadhi ya wananchi ambao wametaka majina yao yahifadhiwe wamesema, mwanamke huyo alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na wanaume wote wawili kwa wakati mmoja jambo lililosababisha kifo Frenk

Wamesema licha ya mauaji hayo kutokea usiku na mwanamke huyo kushuhudia, hakupiga kelele za kuomba msaada wala kutoa taarifa kwa majirani bali alikaa kimya hadi wapita njia walipogundua mauaji hayo jana jambo linalowapa wasiwasi wananchi hao kuwa huwenda mwanamke huyo anafahamu kilichokuwa kikiendelea

By mcharoman

Hakuna maoni: