KIONGOZI mwingine wa kanisa alipatikana amefariki kwenye gesti jijini Nairobi Jumatano usiku chumbani mwake mkiwa na dawa na pombe.
Padri Otto Myer, 70 ambaye ni raia wa Italia, alipatikana amefariki kwenye chumba alichokuwa amekodisha katika the Consolata Guest House mtaani Westlands.
Mwili wa padri huyo ulipatikana kwenye chumba hicho
kando yake kukiwa na dawa, na baadhi ya jirani zake walisema alikuwa akiugua.
Jana, Mkuu wa polisi jimbo la Nairobi, Bw Benson Kibue alisema maafisa wake wanachukulia kifo chake kuwa cha ghafla, hasa kutokana na kwamba amekuwa akiugua kwa siku kadhaa.
“Hatutaharakisha kusema kilichomuua. Kwa sasa tunajua hiki ni kifo cha ghafla, ikizingatiwa kuwa amekuwa akiugua. Upasuaji wa maiti ndio utakaoeleza zaidi kilichomfanya afariki,” akasema Bw Kibue.
Lakini maafisa wa polisi waliofika mahali hapo pamoja na baadhi ya wafanyikazi wa gesti hiyo ambao hawakutaka kutajwa, walisema kwamba chumbani alimokufa padri huyo mlikuwa na dawa pamoja na pombe.
Waliozungumza na Taifa Leo walisema kwamba padri huyo alikuwa ameenda katika hospitali ya karibu kutafuta tiba siku ya Jumanne.
Kifo cha Padri Myer kilitokea saa chache baada ya cha Kasisi Geoffrey Maingi nyumbani kwa mmoja wa washirika wake katika mtaa wa Buruburu, Nairobi.
Sawa na padri Myer, Kasisi Maingi pia alikuwa na umri wa miaka 70 na pia walikufa kwenye vyumba katika hali ya kutatanisha.
Kwenye kisa cha Buruburu, Kasisi Maingi wa kanisa la Redeemed Gospel alisemekana kuegesha gari lake nje ya dua la jumla la Tuskys na kwenda nyumbani kwa mwanamke mshirika, ambaye alikiri kuwa mbali na kuwa kiongozi wake wa kiroho, yeye pia alikuwa rafiki yake.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni